Wednesday, April 24, 2013

RAIS KIKWETE ALIPOKUTANA IKULU NA VIONGOZI WA MADHEHEBU YA KIKRISTO NCHINI TANZANIA



Viongozi wa dini wamewataka waumini kote nchini kulinda amani na umoja uliopo ili nchi isije ikaingia kwenye mgawanyiko wa kidini na kuleta machafuko hapa Tanzania.

Wito huo umetolewa na viongozi wa dini jana Ikulu ya Dar-Es-Salaam mara baada ya kikao cha pamoja baina ya viongozi wa dini na Rais Jakaya Kikwete.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa  jana na
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi, Premi Kibanga,inaeleza kuwa Viongozi hao wa dini walifika jana Ikulu  wakiongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Viongozi wengine walitoka Baraza la Kikristo Tanzania (CCT),Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) na Baraza la Pentekoste Tanzania (PCT).

Mkutano huo ulianza kwa Askofu Ngalalekumtwa kusoma tamko lao la pamoja kwa Rais Kikwete ambalo ndilo lililitoa muongozo wa mazungumzo hayo  ambayo yamehusu Amani na Usalama wa Taifa na migogoro ya kidini ndani ya jamii.

Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo Tanzania ni mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.

“Nataka tuzungumze ni namna gani tunaweza kutoka kwenye hali hii na tunakwendaje mbele zaidi na kuhakikisha nchi yetu bado inakua ya amani na umoja kama ilivyozoeleka” Rais amesema na kutoa nafasi kwa viongozi wa dini kutoa maoni yao.

Viongozi hao wa dini wamemueleza Rais Kikwete kuwa wanaunga mkono jitihada zake za kutafuta amani na kwa pamoja wamekubaliana uandaliwe mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa dini zote ambapo masuala ya amani na umoja wa nchi utajadiliwa kwa kirefu.

Katika kikao cha jana pande zote zimekubaliana kuwa kuna changamoto zilizoko sasa zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuepusha nchi kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi, na pia kukubaliana kuwa pande zote, kwa maana ya serikali na taasisi za dini, zinawajibu mkubwa wa kuhakikisha amani inadumu.


Kabla ya kikao cha hicho , Rais amewahi kukutana na viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo mmoja mmoja ambapo alikua akitafuta maoni na ushauri wa pande zote kabla ya pande zote hazijakaa pamoja na kuwa na msimamo wa pamoja.

Taarifa hiyo imemaliza  kwa kueleza kuwa Kikao cha jana  kimehitimisha jitihada hizo na kinachofuata ni mkutano mmoja ambapo Rais Kikwete atakutana na viongozi wa dini zote kwa pamoja hivi karibuni.

0 comments:

Post a Comment