Saturday, April 6, 2013

Kesi ya mauaji ya padri yaanza

Siku ya ibada ya Mazishi ya Padri Evaristus Mushi aliyepigwa risasi na kufariki mjini Zanzibar 
Na Talib Ussi, Mwananchi  (email the author)

Posted  Aprili6  2013  saa 2:41 AM
Kwa ufupi
Makame aliyegombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Rahaleo mwaka 2010 alifikishwa mbele ya Jaji Mkusa Sepetu jana.

Zanzibar. Mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evaristus Mushi, Omar Mussa Makame (35) mkazi wa Mwanakwerekwe mjini hapa amefikishwa Mahakama Kuu kwa tuhuma za mauaji ya kiongozi huyo wa dini.

Makame aliyegombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Rahaleo mwaka 2010 alifikishwa mbele ya Jaji Mkusa Sepetu jana.
Awali mtuhumiwa huyo alikuwa afikishwe mahakamani Jumanne iliyopita, lakini ilishindikana baada ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Zanzibar kuinyima kibali Polisi kumfikisha mahakamani.
Haikujulikana sababu ya uamuzi huo kwani Mkurugenzi wa Mashtaka, Ibrahim Mzee Ibrahim na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa walitupiana mpira kila mmoja akitaka mwenzake ndiye ataje sababu hizo.
Viongozi hao wote jana hawakupatikana kueleza hatua hii mpya ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo imekuja baada ya uamuzi wa aina gani.
Wakili wa Serikali, Abdallah Issa Mgongo alidai mbele ya Jaji Sepetu kuwa mshtakiwa aliua kwa makusudi Februari 17, mwaka huu eneo la Beit el Rass Wilaya ya Magharibi Zanzibar.
Mgongo alidai tendo hilo ni kosa kwa mujibu wa vifungu 196 na 197 sheria namba (6) za mwaka 2004 ya sheria za Zanzibar.
“Omar Mussa Makame unashitakiwa kwa kosa la kumuua kwa makusudi Padre Evarist Mushi siku ya tarehe 17/02/2013 mnamo saa 12:50 za asubuhi,” alidai Wakili Mgongo.
Makame alikataa kosa hilo la mauaji na wakili wa Serikali aliiomba Mahakama kumrudisha rumande mtuhumiwa hadi hapo ushahidi utakapokamilika.
Upande wa utetezi wakili wa kujitegemea, Abdallah Juma aliiomba Mahakama iamuru ushahidi ukamilike baada ya wiki mbili ili kesi iweze kusikilizwa.
“Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa ni kwamba ushahidi umekamilika nashangaa leo (jana) wakili wa Serikali anasema kwamba bado haujakamilika,” alidai Juma.
Baada ya maombi hayo, Jaji Sepetu alikubaliana na upande wa utetezi na kuwataka mawakili wa Serikali kuharakisha kupeleka ushahidi ili kesi ianze kusikilizwa. Kesi hiyo imepangwa Aprili 18, mwaka huu katika mahakama hiyo.
Mapema Wakili wa upande wa utetezi, Abdallah Juma aliomba mahakama kuanza kusikilizwa ombi lao ambalo walilipeleka Machi 28, mwaka huu ambalo lilitaka kujua kwa nini mteja wao amewekwa ndani kipindi kirefu bila kupelekwa mahakamani.
“Mheshimiwa Jaji kwa heshima yako naomba kwanza tungesikiliza ombi letu halafu tukaja kwenye kesi kwani naona moja inaweza kuharibu nyingine,” alidai Wakili Juma.
Baada ya maombi hayo, Jaji Sepetu alisema hivyo ni vitu viwili tofauti na mahakama haiwezi kukubaliana na maombi hayo.
Jumatano Mahakama Kuu Zanzibar iliamuru kuletwa mahakamani kwa mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evaristus Mushi, Jumatatu ili kuweza kusikiliza shauri lililofunguliwa na mawakili wa upande wa mlalamikiwa la kutokufikishwa mahakamani kwa mteja wao, Makame.
Kampuni ya Uwakili ya AJM Solicitors and Advocate iliwasilisha Mahakama Kuu ya Zanzibar maombi ya Habeas Corpus chini ya kifungu cha 390 cha Sheria ya Makosa ya Jinai sura ya 7 ya mwaka 2007 inayomtaka mtu anayemshikilia mtu mwingine au chombo chochote bila kumfikisha mahakamani kwa saa 24 aieleze mahakama sababu za kumshikilia mtu bila kumfikisha mahakamani au amwachie huru.
Ombi hilo lilikuwa kwa Jaji Mkusa ambaye jana alisikiliza kesi ya kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo.
Padre Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 17, mwaka huu wakati akienda kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Teresia lililopo Beit el Raas nje kidogo ya mjini hapa.

0 comments:

Post a Comment