Saturday, April 27, 2013

Mnyika amshitaki Ndugai kwa wapiga kura wake

Mbunge wa Jimbo la Ubungo wa Chama cha Demokrasia 
na Maendeleo (Chadema), John Mnyika.
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo na Kiongozi wa Kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amemshitaki Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai kwa wapiga kura wake, akiwahoji iwapo walimtuma bungeni kufanya Ubabe wa kuwatoa nje wabunge wenzie badala ya kuwatetea.
Mnyika alitoa Mashitaka hayo jana Aprilli 26, 2013 katika kijiji cha Iyegu, Kata ya Mlali, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, ambapo alisema amemkatia Rufaa Ndugai mara Tano bungeni bila majibu, kwa hiyo jana aliamua kumshitaki kwao ili wafanye maamuzi magumu juu ya mbunge wao asiyefanya kazi waliyomtuma.
Akizungumza katika Mkutano huo Mnyika alimshitaki Ndugai akiwahoji kama walimtuma kufanya hivyo, na waliposema Laa, aliwataka kufanya mabadiliko ya mwakilishi wa Jimbo lao kama wanataka kumaliziwa Kero zao zikiwepo Haki na Maendeleo ya kiuchumi na Matumizi bora ya Rasilimali zao.
Mwananchi mmoja alimhoji Mnyika “Je, ni nani aliyetayarisha, kulinda, kusimamia na kusafirisha Twiga wetu kwenda nje, lini watarejeshwa na waliohusika watafanywaje?.
Mnyika aliwajibu wananchi kwamba, wahusika wa usafirishaji wa Twiga wao ni vigogo walioko madarakani, na Twiga hao wako nchi mmoja ya Kiarabu, na mbali ya Twiga hao hivi karibuni Chadema itaibua suala la Tembo, na kuwaambia suluhisho la haraka kwa yote hayo ni kufanya mabadiliko ya viongozi mafisadi haraka.

Alipoulizwa Mauaji na Vitisho wanavyofanyiwa na Kundi linalojiita Kanyaga Twende, wanapoamua kujiunga na vyama Upinzani, Mnyika aliwauliza kama wanayo simu ya Mbunge wao wamuulize ila wasimtukane, na waliposema hawana aliwatajia namba ya Ndugai na ya Mkurugenzi wa Usalama Chadema ambaye alidai atawawasaidia dhidi ya vitisho .
Aidha Mnyika kabla ya kushuka Jukwani saa 11.30 jioni, aliuuliza umati uliokuwepo uwanjani hapo, wangapi wapo tayari kwa mabadiliko ya M4C, watu wote karibu 1,000 walinyosha mikono na Mnyika akashuka kuelekea Kongwa kuungana na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, kuendelea na Mikutano mingine.

0 comments:

Post a Comment