Friday, April 26, 2013

PROFESA LIPUMBA AIPONDA CHADEMA NA KUDAI KUWA NI VINARA WA VURUGU NA HAWANA HOJA


Chama Cha Wananchi (CUF), kimesema vurugu zinazoendelea bungeni zinasababishwa na Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kushindwa kujenga hoja na mbinu za kuwabana wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema wabunge wa Chadema wana tabia ya kufuata mfumo wa kwenda bungeni na hoja zinazobeba chama chao na si za Watanzania wote kama jinsi CCM wanavyofanya.


“Kambi rasmi ya upinzani imepoteza uwezo wa kujenga hoja za mashiko na mbinu madhubuti za kuwabana wabunge wa CCM bungeni na badala yake Chadema, wamekuwa na tabia mbaya ya kubeba chama chao,” alisema Profesa Lipumba.



Alisema kambi rasmi ya upinzani pia imeshindwa kulinda utaratibu mzuri wa kutetea masilahi ya umma bila jazba na hoja zenye mashiko kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ilipokuwa ikiongozwa na CUF, Kiongozi huyo alisema kambi ya upinzani inapaswa ijipange upya kwa utaratibu na mikakati mizuri ya kuteta hoja za wananchi bila kuyumbishwa na wabunge wa CCM.


“Bunge usiwe uwanja wa kuonyesha mbwembwe za chama bali uwe uwanja wa kutetea haki za wananchi, wabunge wanapaswa wabadilishe mitazamo ya kuona bungeni ni sehemu ya kujionyesha kisiasa na chama chako kinafanya nini nje ya Bunge,” alisema Lipumba.



Alisema viongozi wa Serikali wanapaswa kubadilika kuhusu namna ya kutoa majibu bungeni.


Profesa Lipumba alisema mawaziri wengi wanakuwa wakitoa majibu mepesi katika maswali ya msingi yanayoulizwa na wabunge wa upinzani.


Alisema Bunge linatumia muda na pesa za walipakodi vibaya kwa baadhi ya wabunge kuwa na ubishi usiokuwa na tija, kutoleana matusi na wengine kuingilia hoja za wenzao bila sababu za msingi.


Profesa Lipumba pia alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda amepoteza uwezo wa kuliongoza Bunge.


Mwananchi

0 comments:

Post a Comment