Dodoma/Dar.
Serikali imechukua uamuzi mgumu na kuamua kuwafariji wanafunzi
waliofeli mitihani ya kuhitimu kidato cha nne mwaka 2012 baada ya kufuta
matokeo hayo na kuamua yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu uliotumika
mwaka 2011.
Uamuzi
huo wa Serikali umetokana na matokeo mabaya ya mitihani huo
yaliyosababisha zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi kupata sifuri.
Kutokana
na matokeo hayo, Serikali iliunda Tume inayoongozwa na Profesa Sifuni
Mchome kuchunguza matokeo hayo ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Muda
mfupi baada ya tamko la Serikali, baadhi ya wadau wa elimu wameeleza
kufurahishwa na uamuzi huo, huku Chama cha Walimu Tanzania (CWT)
kikiikosoa hatua hiyo, kuwa imekiuka sheria na kupora madaraka ya Baraza
la Mitihani Tanzania (Necta).
Akitoa
kauli ya Serikali bungeni kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya
Kuchunguza Matokeo ya Mtihani wa Taifa Kidato cha nne mwaka 2012 jana,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), William Lukuvi
alisema wameagiza Necta kuweka viwango ili matokeo ya wanafunzi
yalingane na juhudi zao.
“Standardization
ifanyike ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi wazizoziweka
katika kusoma kwa mazingira, hali halisi ya Tanzania na uamuzi wa taifa
kuongeza idadi ya shule na wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora
unaendelea,” alisema Lukuvi.
Lukuvi
alisema Necta imeelekezwa kuwa licha ya sheria ya kuanzishwa kwake
kuruhusu kufanya marekebisho ya mchakato wa mtihani, marekebisho yoyote
ya kubadilisha utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya
mitihani yanatakiwa yahusishe wadau wote wanaohusika na mitalaa,
ufundishaji na mtihani.
“Wakati
Tume inaendelea kukamilisha kazi yake, uamuzi wa Necta kutumia
utaratibu mpya wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya
mitihani uliotumika 2012 usitishwe,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Badala
yake Necta itumie utaratibu uliotumika mwaka 2011 kwa kidato cha nne na
sita kwa mitihani yote, ikiwamo utaratibu wa Standardization na kutoa
matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo haya.”
Pia,
Serikalli imeagiza mchakato wa tuzo wa taifa (National Qualifications
Framework) na Mfumo wa Kutahiniwa/ kuthamini maendeleo ya mwanafunzi
masomo yake (National Assessment Framework) ukamilishwe haraka
iwezekanavyo.
Katika
mtihani wa mwaka 2012, wanafunzi 367,756 walifanya mtihani huo na
waliofaulu ni 126,847. Waliofaulu kwa kwa madaraja ya kwanza hadi la
tatu ni 23,520 sawa na asilimia 6.4 na daraja la nne ni 103,327 sawa na
asilimia 28.1, huku 240,909 ambao ni asilimia 65.5 wakipata daraja
sifuri.
Kauli ya CWT
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch
alisema Baraza la Mawaziri limepora kazi za Bodi ya Baraza la Mitihani
kwani ndio yenye jukumu la kufuta matokeo kisheria.
Mbali na hilo Oluoch alisema bado wanafanya utafiti ili kuona kama
Baraza la Mawaziri lina uwezo wa kufuta matokeo na kuamuru mitihani
isahihishwe upya, badala ya Bodi ya Baraza la Mitihani.
Oluoch aliyesema tamko rasmi la CWT kuhusu uamuzi huo wa Serikali
litatolewa wiki ijayo, alieleza kuwa kwa sasa wanachunguza kuona kama
jambo hilo lina usahihi kwa kiasi gani.
“Mitihani iliyofutwa ilitolewa na Bodi ya Necta ambayo ndio itakuwa na
jukumu la kusimamia usahihishaji mpya na kutangaza tena matokeo.
Kama hali yenyewe ndio hiyo ni wazi kuwa haina tena uwezo wa kusimamia
jambo hilo, inatakiwa kung’oka na kuundwa bodi mpya,” alisema Oluoch na
kuongeza;
“Nasema hivyo kwa sababu hawawezi kula matapishi yao kwa kuwa wao ndio
wenye mamlaka ya kutoa tena matokeo hayo na walishasema kuwa yalikuwa
mabaya, sasa uzuri wake utatoka wapi tena.”
Alisema kuwa kufutwa kwa matokeo hayo kunaonesha wazi kuwa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeshindwa kazi ya kusimamia elimu nchini.
“Pia katika utangazaji wa matokeo anatakiwa waziri mpya wa kufanya hivyo
kwa kuwa huyu wa sasa alieleza sababu za wanafunzi kufeli, sasa akiwa
anatangaza matokeo mapya atatueleza nini,” alihoji.
Sababu za matokeo mabaya
Waziri Lukuvi alisema takwimu zinaonyesha kushuka kwa ufaulu huo unahusu
shule zote na asilimia kwenye mabano, shule za wananchi (1.82); Shule
za umma yaani kongwe (6.43); Binafsi (6.39) na Seminari (7.29).
Kuhusu matokeo ya kidato cha nne 2012, Lukuvi alisema tume imebaini
licha ya wanafunzi kuwa kwenye mazingira yanayofanana na wenzao
waliopita, ufanisi umekuwa ukishuka kwa sababu mbalimbali.
“Ufaulu wao umeshuka zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya mchakato wa
kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani mwaka 2012, mfumo uliotumika kupanga
matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika miaka iliyotangulia,”
alisema Lukuvi na kuongeza:
“Uchunguzi unaonyesha kuwa mwaka 2011, Necta lilikuwa linachakata alama
za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kutegemea hali ya
ufaulu kwa mwanafunzi ambao ni National Mean Difference (NMD).
Alisema uataribu huo ulitokana na tofauti ya wastani wa kitaifa wa alama
za maendeleo, kutoka alama ya maendeleo endelevu (Continued
Assessment-CA) za watahiniwa wote na wastani wa kitaifa wa ufaulu wa
mtihani wa mwisho kwa somo husika.
Aliendelea kuwa kila mtahiniwa aliongezewa NMD iliyokokotolewa kwenye
alama za mtihani wa mwisho, ili kupata alama itakayotumika kupada daraja
la ufaulu.
“Lakini mwaka 2012 lilitumia mfumo mpya wa kuwa na viwango maalumu vya
kutunuku (Fixed Grade Range). Tume imebaini kwamba licha ya mfumo huo
ulioandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya hakufanyiwa utafiti wa
maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika,” alisema.
Lukuvi alisema taarifa ya awali ya tume, inaonyesha kutokana na
uchunguzi uliofanyika kwa muhtasari imebaini mambo mbalimbali.
Alisema matokeo ya kidato cha nne kuanzia mwaka 2008 yamekuwa na
mserereko wa kushuka tofauti na miaka iliyotangulia, kwa sababu ya
changamoto zinazotokana na mafanikio yaliyopo sasa ya kuongezeka kwa
idadi ya shule za msingi na sekondari, hususan mwaka 2011 na 2013 hivyo
kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi.
“Mwaka 1961 hadi 2011 idadi ya wanafunzi kwa shule za msingi imeongezeka
kutoka 486,470 hadi 4,875,764, sawa na ongezeko la wanafunzi 4,389,294
kwa takriban miaka 40,” alisema.
Alisema wanafunzi wameongezeka kutoka 4,875,764 mwaka 2001 hadi
8,247,472 mwaka 2012, sawa na ongezeko la wanafunzi 3,371,708 kwa
kipindi cha miaka 11.
Sekondari wanafunzi wameongezeka kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 289,699
mwaka 2001 sawa na ongezeko la wanafunzi 274,867 kwa miaka 40.
Lukuvi alisema kati ya mwaka 2001 hadi 2012 wanafunzi wameongezeka
kutoka 289,699 hadi 1,884,270 sawa na ongezeko la watu 1,594,571.
Tume hiyo imebaini changamoto nyingine ni mazingira yasiyo ya kuridhisha
ya kufundishia na kujifunzia, ikiwamo upungufu wa miundombinu muhimu ya
shule; madarasa, madawati, maktaba, nyumba za walimu, bweni na majengo
mengine muhimu.
“Kuna tatizo la uhaba wa walimu, vitabu, zana za kufundishia na matatizo
ya ukaguzi wa shule. Vilevile tumebaini Mfumo wa Elimu ya Msingi na
Sekondari unakabiliwa na changamoto nyingine mbalimbali ambazo taifa
linapitia kwa sasa,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Yapo masuala ya sera, sheria,
mfumo, muundo na changamoto za uhaba wa rasilimali fedha na watu. Tume
inaendelea kufanyia kazi maeneo haya kwa kushirikiana na wataalamu na
wadau wengine.”
source: Mwananchi
Winstar Casino and Resort - Jackson, MS - Jackson, MS
ReplyDeleteFind out more about the Winstar Casino and Resort, 익산 출장샵 including room types, restaurants and 안동 출장샵 amenities, maps, photos, 안산 출장마사지 videos, address, telephone 부산광역 출장마사지 number, 시흥 출장샵