Saturday, May 4, 2013

AJALI YAUA ZAIDI 5 WENGINE ZAIDI YA 20 WAJERUHIWA VIBAYA IRINGA JANA JIONI



 Moja kati ya ajali ya basi la Taqwa (picha na maktaba yetu)
.......................................................

Abiria zaidi watano waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Taqwa lenye namba za usajili T 273 CDR kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Malawi wamekufa papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyotokea jioni hii katika eneo la Nyololo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Akizungumza na mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com mmoja kati ya mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Dkt Matatala alisema kuwa ajali hiyo imetokea mida ya saa 11 jioni wakati basi hilo likitokea Dar es Salaam kwenda nchini Malawi.

Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori lenye namba za usajili T 104 DZZ ambalo lilikuwa likitokea Makambako kuelekea Iringa,lori lililokuwa likijaribu kulipita lori lenye namba za usajili T 227 AVC na kushindwa kupita na kuishia kugongana uso kwa uso na basi hilo ambalo pia lilikuwa likija kwa mwendo wa kasi.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo wamesema kuwa ajali hiyo imetokea katikati ya mji wa Nyololo ambapo ni jirani kabisa na eneo lenye matuta ya kuzuia magari kwenda kwa mwendo kasi.

 Alisema kuwa hadi majira ya saa 12.45 jioni maiti tano zilikuwa zimetolewa katika basi hilo la Taqwa na kuwa jitihada za wasamaria wema kutoa maiti na majeruhi katika eneo hilo zimeendelea kufanyika.

Mbali ya maiti hizo pia alisema jumla ya majeruhi 20 waliokolewa na kukimbizwa katika Hospitali ya wilaya ya Mufindi kwa matibabu zaidi. Dkt Matatala alisema kuwa katika tukio hilo wananchi wameweza kuimarisha ulinzi zaidi katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kulinda mali za majeruhi na abiria waliopoteza maisha yao kwa ajili hiyo.

Wakati huo huo wananchi wa eneo hilo la Nyololo wameelekeza lawama zao kwa jeshi la polisi wilayani Mufindi kwa kuchelewa kufika katika eneo la tukio na kuwa taarifa wamepewa mapema ila hadi majira ya saa 12.50 hakukuwepo na askari aliyefika eneo hilo.

Hii ni ajali ya pili kutokea katika wilaya ya Mufindi kwa kipindi cha wiki moja baada ya ajali nyingine mbaya kama hii kutokea eneo la Mafinga kwa gari ndogo iliyokuwa ikiendeshwa na paroko wa kanisa katoliki Ifunda marehemu Alfonce Mhamilawa kutokea kwa kuingia nyuma ya lori. 
CHANZO; http://www.matukiodaima.com/

0 comments:

Post a Comment