Wednesday, March 13, 2013

makundi yaibuka mchakato wa kumchagua papa

Wednesday, March 13, 2013

Makundi yaibuka mchakato wa Papa

Vatican City. Dirisha limefunguliwa tayari kwa hewa safi kuingia Vatican City. Hivi ndivyo unavyoweza kuuelezea mchakato wa kumpata Papa wa 226 wa Kanisa Katoliki, unaoanza leo.
Mchakato huo unaanza rasmi saa 10.45 jioni kwa saa za Vatican (Saa 12.45 kwa saa za Afrika Mashariki) na utatanguliwa na ibada maalumu ya misa ya makadinali 115 wanaoshiriki katika uchaguzi huo.
Tayari, vumbi limeanza kutimka huku makundi makubwa matatu yakiibuka katika uchaguzi huo, unaofuatiliwa kwa karibu kote duniani na ambao unaweza kudumu hadi wiki mbili.
Makundi hayo ni pamoja na lile la makadinali wa Italia, wapatao 28 dhidi ya Wamarekani 11, wote wakiwa na malengo tofauti katika nia yao ya kuchukua wadhifa huo wa juu katika Kanisa Katoliki.
Hata hivyo, Italia ina mgawanyiko mkubwa wa vikundi vya kiitikadi miongoni mwa waumini wake, kama ilivyo kwa makadinali hao, jambo ambalo linapunguza umoja wao.
Wataliano kwa upande mwingine, wangependa kumaliza miaka 35 ya utawala wa wageni katika Vatican tangu alipoingia Papa Yohane Paul II mwaka 1978 (sasa mwenyeheri) na mfuasi wake, Benedict XVI na hivyo kurejesha miaka zaidi ya 450 ya utawala wao katika kiti hicho cha Mtakatifu Petro, wakipenda pia kudumisha mazoea ya utawala wa kirasimu katika uongozi huo.
Tofauti na miaka ya nyuma, wachambuzi wa masuala ya dini na imani, wanaona kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni mwepesi zaidi kwani hakuna kadinali mwenye nyota zaidi ya wengine miongoni mwa washiriki hao 115, ambao angepewa nafasi kubwa kuibuka mshindi.
Hata hivyo, Wamarekani, taifa kubwa na tajiri duniani wanaowakilishwa na makadinali 11, imani yao ni kutaka kuupeleka nchini mwao, uongozi wa Vatican. Dhamira yao, pia inapingwa.
Hao wanadhani kuwa Marekani haiwezi kutoa kiongozi mkuu wa kanisa hilo, ambaye ataweza kukabiliana na wapinzani wa Ukristo na kuaminika kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Kundi lingine na ambalo linaweza kubadili matokeo, ni la wateule 67 wa Papa Benedict ambao ni zaidi ya nusu ya wapigakura wote.
Wao wanaelezwa kuwa mchango wao katika uchaguzi huo utakuwa mkubwa na hata kuathiri matokeo, kama watapenda kuendeleza misingi ya uongozi wake.
Pamoja na makundi hayo, kuna baadhi ya makadinali ambao kura ya maoni, imeendelea kuwabeba zaidi kabla ya uchaguzi wenyewe kuanzia leo.

0 comments:

Post a Comment