Wednesday, March 13, 2013

MAKALA: MWIMBAJI NYOTA AMBAYE JARIBIO LA MAMA YAKE KUTOA MIMBA YAKE ILISHINDIKANA

MAKALA: MWIMBAJI NYOTA AMBAYE JARIBIO LA MAMA YAKE KUTOA MIMBA YAKE ILISHINDIKANA

Fred Hammond.                    ©chan-lo
Leo katika makala kadomole blog imeamua kukanyaga ardhi ya Marekani ambako kuna idadi kubwa ya waimbaji wa muziki wa injili ambao wanafahamika sana karibu dunia nzima na mmoja kati ya waimbaji hao ni Fred Hammond baba wa watoto wawili ambaye historia yake katika muziki wa injili inafahamika vyema. Mwimbaji huyu alizaliwa tarehe 27/12/1960 anasifika kwa upigaji mahiri wa gitaa la bass, mwimbaji pia ni mtayarishaji mzuri wa muziki ama kwa kimombo wanasema Producer.
Mwimbaji huyu anayefanya kazi chini ya lebo ya kurekodia ya Verity Records ameshiriki katika makundi mbalimbali ya gospel kama The Winans, Commissioned na kundi lake la Radical For Christ akiwa amejinyakulia tuzo za Grammy, Dove, Stellar lakini pia jina lake limewahi kupendekezwa katika tuzo mbalimbali. Katika maisha yake yote mwimbaji huyu hakuwahi kuweka hadharani siri nzito kuhusu mama yake mzazi ambaye kwasasa ni marehemu.
Kupitia katika kipindi cha mahojiano na mwimbaji mwingine mkongwe Donnie McClurkin, Fred amesema wakati mama yake akiwa na ujauzito wake alijaribu kutoa bila mafanikio.
Amesema mama yake alikwenda kliniki kwa lengo la kutoa mimba yake ambapo kwa wakati huo miaka ya 50 hadi miaka ya 60 ilikuwa ni kosa utoaji wa mimba lakini alikwenda kwa kificho na kufanikiwa kufanya kile alichokitaka kuharibu mimba hiyo ambapo aliambiwa arudi nyumbani ambako mtoto angetoka kisha angemweka kwenye begi kumrudisha hospitali, ambapo kwa mujibu wa mwimbaji huyo amesema mama yake alidhani alifanikiwa lengo lake kwakuwa alitokwa na damu na alipofika nyumbani kwa siku tatu mfululizo hakuna chochote kilichotokea. 
Akaamua kurudi tena kliniki na kuwaambia kwamba hadhani kama lengo lilifanikiwa na walipomcheki wakagundua ni kweli angali bado akiwa na mtoto hai tumboni ambapo watu hao wakamwambia siku hiyo ingewezekana kabisa kuitoa mimba hiyo na kumwambia alale kitandani tayari kwa zoezi hilo ambalo tayari kwa wakati huo watu hao walishashika vifaa kuanza kazi hata hivyo mama huyo aliamua kubadili mawazo na kuamka haraka kutoka kitandani hapo na kuvaa nguo zake kwakuwa alipata hisia ndani yake kwamba angekufa pale kitandani endapo angefanya kitendo hicho cha utoaji mimba.
Siri hii alipewa mwimbaji huyo ikiwa ni miezi mitatu kabla ya mama yake mzazi kufariki dunia, ambapo amesema ndio maana yeye hataki kuchezea huduma ya Mungu na kwamba Mungu alikuwa na makusudi naye kwani wakati mama yake alipotaka kutoa mimba yake, yeye mwenyewe (Mungu) alimwepusha na hilo na hata katika maisha aliyoishi toka wakati huo Mungu huwa anamshindia katika kila kitu. Usione Fred Hammond anaimba hiyo ni moja ya sababu inayomfanya kumpazia sauti za sifa Mungu wake aliyemuepusha na kifo.

0 comments:

Post a Comment