Profesa Tibaijuka achangia sh. mil. 46 ujenzi kanisa Katoliki Kitunda
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amechanga sh. Mil. 46 kwa
ajili ya ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kitunda, Jimbo Kuu la Dar
es Salaam.
Profesa Tibaijuka aliyekuwa mgeni
rasmi katika harambee hiyo, Rais wa Awamu ya Tatu, Wiliam Benjamin Mkapa
ambaye hakuwepo katika harambee hiyo alichangia sh. Mil. moja katika ya
sh. mil. 95 zilizochangwa.
Katika harambee hiyo ambayo jiwe la
msingi liliwekwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama
Policarp Kardinali Pengo aliyewakilishwa na Katibu Mkuu wa Baraza la
Maaskofu Tanzania, Padri Raymond Sabba, Profesa Profesa Tibaijuka
alimsifu Askofu Pengo kuhamasisha ujenzi wa makanisa ya kisasa na
kuongeza huduma za kiroho kwa waumini kufikia parokia 79 za Jimbo la Kuu
la Dar es Salaam.
Waziri alisema Serikali inafarijika
kuona watanzania wanaishi maisha yenye utulivu na kuwapongeza viongozi
wa dini kuendelea kutoa huduma za kiroho kwa waumini wao.
Alisema miji mingi duniani imeendelea
kutokana na wananchi wake kuwa na nidhamu na kuongeza kuwa ongezeko la
ukuaji wa kasi wa miji mingi hapa nchini ni changamoto kwa wizara yake
kuhakikisha upimaji unafanyika.
Kanisa la Kitunda litakalogharimu sh.
Bil. 1.5 mpaka litakapokamilika katika risala yao iliyosomwa na katibu
wa Baraza la Walei Parokia ya Kitunda, Bw. Simon Nguka ilisema
wanakabiliwa na changamoto nyingi mojawapo ni urasimu wakati
wanafuatilia hati miliki ya eneo la kanisa hilo.
Profesa Tibaijuka alisifu ukubwa wa
kanisa hilo na ramani yao ya kisasa na kuahidi kuwa upimaji wa nyumba za
wakazi wa eneo hilo utaanza karibuni na kuwaomba wanananchi watoe
ushirikiano kazi hiyo itakapokuwa imeanza.
Alisema upimaji utakapoanza kama kuna
nyumba za kuabudia zitakuwa zinahitajika kuongezewa eneo wananchi wa
nyumba jirani watoe ushirikiano wa kupisha maeneo hayo.
Katika mahubiri ya Padri Sabba
aliyeongoza ibada ya misa takatifu aliwaomba waumini wa Parokia ya
Kitunda kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa
kanisa hilo.
mwisho